Monday, May 18, 2015

Septena To The Holy Spirit

For the swahili speakers - you can use this text (which copyright for swahili edition I own) freely for the sake of your community, liturgy or your private use.



Septena kwa Roho Mtakatifu kabla ya Sherehe ya Pentekoste
Hekalu la Huruma ya Mungu, Kiabakari, Jimbo la Musoma

Kuanzia siku ya Sherehe ya Kupaa Bwana hadi Jumamosi kabla ya Sherehe ya Pentekoste, septena kwa Roho Mtakatifu huadhimishwa (badala ya novena kama iliyokuwa zamani kutokana na kuhamishwa kwa Sherehe ya Kupaa Bwana kutoka Alhamisi kabla ya Dominika ya 7 ya Pasaka kuchukua nafasi ya Dominika ya 7 ya Pasaka; hivyo siku zinazofuata Sherehe ya Kupaa Bwana kupungua na kubaki saba tu). Septena huanza Jumatatu baada ya Sherehe ya Kupaa Bwana na kumalizika katika Vijilia ya Sherehe ya Pentekoste.

MFANO WA KWANZA: Inashauriwa Septena kwa Roho Mtakatifu iadhimishwe kwa Liturujia ya Masifu ya Jioni. Mama Kanisa hupendelea njia hii ambayo kwayo Sala ya Kanisa zima hupaa kwa Roho wa Bwana kuomba aje na mapaji yake; aidha ni Liturujia inayomfanya mwamini atafakari Uwepo wa Roho wa Bwana katika maisha yetu. Kwa njia ya nyimbo, antifona, zaburi, somo, viitikizano na maombi tunamwomba Roho Mtakatifu tukiungana  na Kanisa zima linalosali kwa njia ya Masifu ya Jioni. Masifu haya yanaweza kuunganishwa na Adhimisho la Misa Takatifu saa za jioni.

MFANO WA PILI: Kama mazingira hairuhusu kuadhimisha Masifu ya Jioni, basi, sala zilizopendekezwa hapo chini, zisaliwe wakati wa Misa za asubuhi au wakati wa Ibada za Bikira Maria mwezi wa Mei au Ibada za Moyo Mtakatifu mwezi wa sita.


Jumatatu na Alhamisi

Ee Bwana Yesu Kristo! Siku ya Kupaa kwako mbinguni uliwaamuru Mitume wako wasiondoke Yerusalemu, bali waingoje Ahadi ya Baba. Uliwaambia: ‘Yohane alibatiza kwa maji, lakini ninyi muda si mrefu mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu…Roho Mtakatifu atakapowashukia, mtapewa Nguvu zake na mtakuwa mashahidi wangu mpaka miisho ya dunia’ Kwa mfano wa Mitume, ambao pamoja na Maria, Mama yako, na wanafunzi wako wengine, walidumu kwa moyo mmoja katika sala, wakiingoja Ahadi ya Baba, vivyo hivyo na sisi wenyewe tunatamani kujiandaa kwa njia ya sala za pamoja kwa ajili ya Ujio wa Roho Mtakatifu. Tunasadiki kwamba ndiye Yeye anayelishukia Kanisa lako katika nyakati zote, hutushirikisha karama zake, hulihuisha Kanisa na kulipenyeza kwa Nguvu zake na Upendo wake. Tunasadiki kwamba ndiye Yeye anayemdhihirisha Mungu kwa ulimwengu, ndiye Yeye anayekudhihirisha Wewe, Bwana na Mkombozi kwetu na kwa wanadamu wote.

Tunatamani kushirikishwa Nguvu za Roho Mtakatifu na kwa njia ya Nguvu hizo kugeuka kuwa Mashahidi wako katika familia zetu, jumuiya zetu, parokiani, Jimboni, katika nchi yetu na kokote utakakotutuma. Ndiyo maana tunakuomba kwa matumaini na unyenyekevu:

Utushushie Roho wako Mtakatifu, ee Bwana!
  • Bwana Yesu, uliye Ukweli, Hekima na Mwangaza wa Baba, utushushie mwanga na ukweli wako, tuweze siku zote – kwa neno na tendo – kukushuhudia Wewe mbele ya watu wote.
  • Roho wako Mtakatfiu atuongoze, tuweze kuishi na kutenda daima kama watoto wa Mungu.
  • Uyafunulie mataifa yote Injili yako, ili watu wote wapate kuitii imani ya kweli.
  • Utushushie Roho Mtakatifu, tuweze kukiri mbele ya mataifa kwamba Wewe ndiwe Mfalme na Bwana wao.
  • Utujalie ili mwenendo wa kila mmoja wetu uwavutie watu wote kwako na kuwaletea faida ya kiroho na kimwili.
  • Tunaomba Roho wako aje kwetu na kwa ukarimu wake wa daima aiongoze historia ya ulimwengu akiifanya upya sura ya nchi.
  • Uwaongoze kwa nuru ya Roho wako wale wote wanaotutawala, wawe watumishi wako waaminifu kwa manufaa ya wananchi wote.
  • Wewe, ambaye siku ya Pentekoste uliyaalika mataifa yote yaliyotawanyika duniani yaingie katika Familia moja ya Kanisa lako, utujalie kwa nguvu ya Roho wako Mtakatifu ili ulimwengu wote uungane katika imani moja ya kweli.

Na sasa tusali kama alivyotufundisha Bwana wetu Yesu Kristo: Baba yetu…

Tuombe: Tunakuomba, ee Mungu Mwenyezi, Roho Mtakatifu atuwashe kwa moto ule ambao Bwana wetu Yesu Kristo aliushusha uliwenguni akitamani uwake kwa nguvu zote. Anayeishi na kutawala daima na milele. Amina.


Jumanne na Ijumaa

Bwana wetu Yesu Kristo! Wakati wa Karamu ya Mwisho, uliwaahidi Mitume, waliohuzunika kwa sababu uliwaambia habari za kutoka kwako katika ulimwengu huu baada ya muda si mrefu, kwamba utamtuma kwao Roho Mtakatifu Mfariji. Uliwaambia: ‘Nitamwomba Baba naye atawapa Msaidizi mwingine, ali awe nanyi daima – Roho wa Kweli, ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa sababu haumwoni wala haumjui. Lakini ninyi mnamjua, maana hukaa miongoni mwenu na atakaa ndani yenu’. Ahadi yako, Yesu, ilipata kutimia: Roho Mtakatifu siku ya hamsini baada ya Ufufuko wako alilishukia Kanisa na kubaki ndani yake daima. Roho wako hulijaza Kanisa, huliongoza, huliunganisha na kuliimarisha, akiendelea kulishukia daima katika Sakramenti za Kanisa, hugeuza mkate na divai kuwa Mwili na Damu yako na kuwatakatifuza wote wanaokupokea katika Ekaristi kwa moyo safi. Roho Mtakatifu analifanya Kanisa lako kuwa jipya daima. Tunasadiki kwamba Roho huyo huyo yu miongoni mwetu. Tunasadiki kwamba Roho Mtakatifu aliyefanya makao yake katika utu wako mtakatifu, hukaa pia ndani mwetu na kutuunganisha nawe na Baba, hutufanya kuwa mwili mmoja. Tunakuomba neema zake ziendelee kulitakatifuza Kanisa lako daima na kutuongoza hadi kwenye umoja kamili na Baba. Ndiyo maana tunakuomba:

Ututakatifuze katika Roho Mtakatifu, ee Bwana Yesu!

  • Utushushie Roho wako, ee Bwana, ili Kanisa lako liendelee kuhuishwa na kufanywa jipya daima.
  • Uwatazame wote wanaojiita wakristo, ili Roho Mtakatifu awaunganishe katika kundi moja chini ya mchungaji mmoja.
  • Yesu Kristo, Mchungaji wa milele, uwajalie hekima na busara wachungaji wetu, ili wawaongoze wanakondoo wako katika njia za wokovu kwa ufanisi mkubwa.
  • Utujalie tusiongozwe na roho ya ulimwengu huu, bali na Roho wako Mtakatifu anayetoka kwako.
  • Ulijalie Kanisa lako Roho wa Umoja, kusiwepo tena miongoni mwetu na utengano, chuki na uadui.
  • Utujalie nguvu za Roho Mtakatifu, aweze kututakasa na kutuimarisha.
  • Uwaandae kwa neema ya utakaso wale wote wanaojiandaa kuzipokea karama za Roho wako Mtakatifu katika Sakramenti ya Kipaimara.
  • Utujalie upendo wa kweli, tuzidi kupendana kindugu.

Na sasa tusali kama alivyotufundisha Bwana wetu Yesu Kristo: Baba yetu …

Tuombe: Ee Mungu, uliyemtuma Roho Mtakatifu kwa Mitume wako, usikilize maombi yetu tunayokutolea kwa matumaini, na jinsi ulivyotujalia neema ya imani, utujalie pia amani na umoja. Kwa njia ya Kristo, Bwana wetu. Amina.


Jumatano na Jumamosi

Bwana wetu Yesu Kristo! Wakati ule ulipaaza sauti katika Hekalu la Yerusalemu na kuwaalika watu wako: ‘Aliye na kiu na mwenye kuniamini – aje kwangu anywe! Jinsi Maandiko yasemavyo: Mito ya maji ya uzima itabubujika ndani mwake’. Na hayo uliyasema juu ya Roho Mtakatifu, ambaye wale wanaokuamini na kukufuata walikuwa wampokee. Katika kila mmoja wetu, aliyetakaswa kwa maji ya Ubatizo, mwujiza huo huo hujirudia: chemchemi ya uzima wa milele hububujika kutoka ndani ya kilindi cha roho zetu. Chemchemi hiyo ni Roho wako Mtakatifu. Ndiye Yeye anayetuangaza kwa nuru ya imani, huamsha matumaini ya ufufuko, humimina upendo ndani ya mioyo yetu. Kutoka wingi wa ukarimu wake twapokea mapaji yake saba ambayo utimilifu wao huonekana kwako, ee Yesu. Kutoka katika neema zake fadhila zote na matendo mema hupatikana, ndiyo matunda ya Roho Mtakatifu: upendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, upole, uaminifu, kiasi. Ndiye Roho Mtakatifu anayetufundisha kusali, ‘maana tusipojua kusali jinsi inavyotupasa, Roho mwenyewe hutusaidia katika maombi ambayo hayawezakani kuelezwa kwa maneno ya kibinadamu’. Utakatifu wetu wote, ufanano wetu binafsi na Yesu - mwanzo wake umo ndani yake Roho Mtakatifu anayeishi ndani mwetu. Ndiyo maana, tukisadiki hayo, tunakuomba:

Ututakatifuze katika Roho Mtakatifu, ee Bwana Yesu!
  • Neno lako, ee Kristo, likae kwa wingi wake ndani mwetu, tuweze daima kukupa shukrani zetu katika zaburi, nyimbo na tenzi za kiroho.
  • Ulitufanya kuwa watoto wako kwa njia ya Roho Mtakatifu; utujalie tumuabudu Mungu Baba kwa njia yako katika Roho huyo huyo. 
  • Utujalie hekima katika maamuzi na matendo yetu, ili tufanye yote kwa utukufu wa Mungu.
  • Utujaze furaha na amani katika imani yetu, tujazwe wingi wa matumaini na nguvu za Roho Mtakatifu.
  • Utufanye kuwa kitu kimoja na Roho wako, ili dhiki, shida na matatizo mbalimbali visitutenganishe nawe kamwe.
  • Umtume Roho wako, Mgeni mpendwa wa roho zetu, na utujalie tusimhuzunishe kamwe kwa njia yoyote ile. 
  • Ee Bwana, unayefahamu kilichomo ndani ya kila mmoja wetu, utuongoze daima katika njia za ukweli na uwazi.
  • Utujalie neema, tusiwahukumu wenzetu wala kuwadharau, kwa maana sote tutasimama siku ya hukumu mbele yako.
  • Umtume Roho Mtakatifu, Nuru Takatifu isiyofikika, aijaze mioyo yetu.

Na sasa tusali kama alivyotufundisha Bwana wetu Yesu Kristo: Baba yetu …

Tuombe: Ee Mungu Mwenyezi, tunakuomba utujalie ituangaze nuru ya Utukufu wako, naye Roho Mtakatifu kwa mwangaza wake aimarishe mioyo ya wale waliozaliwa upya kwa njia ya Neema ya Ubatizo. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.





SIKU YA MWISHO YA SEPTENA
IBADA YA VIJILIA YA SHEREHE YA PENTEKOSTE



Ibada ya Vijilia ya Sherehe ya Pentekoste hutusaidia kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya Adhimisho la Sherehe hiyo. Ibada hii huadhimishwa saa za jioni siku ya Jumamosi kabla ya Sherehe ya Pentekoste. Sehemu mbili muhimu za Ibada hiyo ni Kumbukumbu ya Mashahidi wa Imani na Ibada ya Kurudia Utume wa Waamini unaotokana na Kipaimara.

Ibada ya Kuanzia

Wimbo wa mwanzo huimbwa (wimbo wa Roho Mtakatifu). Wakati huo Kiongoza-Ibada akitanguliwa na Watumishi wa Altare na Wahudumu wa Neno la Mungu hufika altareni na kutoa heshima kama kawaida wakati wa Ibada ya Neno la Mungu (huinama mbele ya altare lakini haibusu altare). Huanza ibada kwa ishara ya msalaba na kuwasalimu waamini kwa salamu ya kiliturujia kama kawaida (Bwana awe nanyi…  au Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo….). Kisha hutoa neno la utangulizi akitumia maneno yafuatayo au yanayofanana na hayo:

Ndugu zangu wapendwa! Tunashangilia Ushindi wa Bwana wetu Yesu Kristo aliyefufuka! Tunafurahia matunda ya Ushindi wake! Na kwa nguvu ya Ushindi huo, kwa imani ya Kanisa inayotufundisha kwamba Yesu Kristo aliyeteswa na kuuawa msalabani akafufuka siku ya tatu, vizazi kwa vizazi vya wafuasi wake walijawa ujasiri wa kuikiri imani hiyo ya Kanisa katika dhiki na taabu za kila namna. Jioni hii ya leo, tunapoadhimisha Ibada hii ya Vijilia ya Sherehe ya Pentekoste na kwa njia hiyo kujiandaa vema kuamsha mapaji ya Roho wa Bwana tuliyopewa siku ya Ubatizo wetu na katika Sakramenti ya Kipaimara, na kuzipokea karama mpya mbalimbali  za Roho wa Bwana, tunapenda kutambua uwepo wake na kazi zake katika Kanisa la Kristo. Tunapenda kukutana na ndugu zetu katika imani ambao hawakusita kuutoa uhai wao kwa ajili ya imani ya Kanisa. Tunapenda kuwakumbuka mashahidi wa imani  walioihubiri Injili ya Bwana mpaka kumwaga damu yao kwa ajili ya Jina la Bwana. Kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao na kifo chao kwa ajili ya Kristo, walikiri imani hadi pumzi yao ya mwisho, wakamshinda Yule Mwovu na kuchangia kwa kiasi kikubwa kushinda mitandao ya uovu katika ulimwengu tunamoishi. Basi, mashahidi wa Bwana, ndugu zetu katika imani moja, watusaidie kwa maombezi yao nasi tukiri imani ya Kanisa kwa ujasiri tukimshuhudia Kristo Mfufuka katika maisha yetu ya kila siku, katika hali zote na mahali popote tunapoishi na kufanya kazi.

Kiongoza-Ibada anasali sala ya Kolekta:

Tuombe: Ee Mungu, unayeongoza historia ya wanadamu katika njia za wokovu, tunakuomba kwa unyenyekevu, utuepushe na yote yanayoweza kutudhuru katika safari ya wokovu na kutujalia mema yote tunayohitaji katika maisha yetu ya kumshuhudia Kristo Mfufuka kwa ujasiri na bidii kubwa. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele. Amina.

Liturujia ya Neno


Somo la Kwanza: 1 Pet 1,3-9.13-21
Wimbo wa Katikati: Ap 19,1c-2a.5b.7
Somo la Pili: Ebr. 12,1-6.18-19a.22-24
Shangilio: Yn 12,24-25
Somo la Injili: Mt 5,1-12


Kiongoza-Ibada hutoa homilia baada ya Somo la Injili. 


Kumbukumbu ya Mashahidi wa Imani

Kiongoza-Ibada  huwaambia waamini yafuayato au yanayofanana na hayo:

Ndugu zangu! Baada ya kulipokea Neno la Mungu na kulitafakari kwa pamoja; Neno, ambalo kwa wengine ni lugha ngumu na kwa wengine ni Neno la Uzima na taa ya miguu yao, tufungue sasa mioyo yetu na akili zetu, tuzipokee shuhuda za wale waliofaulu kulipokea Neno hilo na kulitafakari mioyoni mwao na kuliishi kwa ushujaa hadi kumwaga damu yao. Shuhuda za maisha yao zituimarishe sisi wenyewe na kututia moyo wa kuiga mfano wa maisha yao katika maisha yetu sisi wenyewe na kumshuhudia Yesu Mfufuka kwa ujasiri bila woga.

Kiongoza-Ibada mwenyewe au msomaji aliyeandaliwa husoma historia fupi za wafiadini au watakatifu wachache (au waamini marehemu wanaosifika kwa maisha yao ya uchaji wa Mungu katika mazingira ya mahali pale).


Kurudia Ahadi za Ubatizo

Kiongoza-Ibada huwakaribisha waamini wasimame na kuwasha mishumaa yao kutoka kwa mshumaa wa Pasaka. Kisha anaeleza yafuatao:

Wapendwa, tukishika mishumaa iliyowashwa kwa mara ya kwanza siku ya Ubatizo; mishumaa tuliyoahidi kutunza mwanga wake hadi saa ya kufa kwetu; turudie sasa Ahadi zetu za Ubatizo. Kumkataa Shetani na kukiri imani yetu kuwe ni ishara ya utayari wetu wa kwenda kuhubiri Habari Njema kwa watu wote na kuwashirikisha imani iliyo utajiri na nguvu ya maisha yetu. Hivyo basi, mbele ya Mwenyezi Mungu aliye Shahidi wa Ibada yetu, na mbele ya Kanisa, ninamuuliza kila mmoja wenu:

Mwamkataa Shetani? Namkataa.
Na mambo yake yote? Namkataa.
Na fahari zake zote?  Namkataa.

Mwasadiki kwa Mungu Baba Mwenyezi, Muumba mbingu na dunia? Nasadiki.
Mwasadiki kwa Yesu Kristo, Mwanae wa pekee, Bwana wetu, aliyezaliwa na Bikira Maria, akateswa, akafa, akazikwa, akafufuka katika wafu, amekaa kuume kwa Baba? Nasadiki.
Mwasadiki kwa Roho Mtakatifu, Kanisa takatifu katoliki, ushirika wa Watakatifu, maondoleo ya dhambi, ufufuko wa miili na uzima wa milele? Nasadiki.

Hiyo ndiyo imani yetu. Hiyo ndiyo imani ya Kanisa tunayoona fahari kuiungama katika Yesu Kristo Bwana wetu. Amina.

Kiongoza-Ibada huwarashia waamini wote maji ya baraka. Wote huimba wimbo ufaao.


Sala ya Waamini

Kiongoza-Ibada huwaalika waamini kutoa maombi kwa maneno yafuatayo:

Sisi, wafuasi wa Yesu Mfufuka, tunataka kuiga mfano wa wafuasi wa kwanza wa Bwana, tukibeba mioyoni mwetu nuru ya imani yetu kwa Kristo, aliyekufa msalabani na kufufuka kwa ajili ya wokovu wetu; tunataka kwa makusudi mazima, kwa bidii na ujasiri kupeleka mbele ya kiti cha enzi cha Mungu Baba Mwenyezi mastahili ya mashahidi waaminifu wa Bwana, ndugu zetu katika imani, pamoja na mateso yetu, misalaba na shida mbalimbali, hatari za kimwili na za kiroho. Sala yetu hii ituimarishe katika safari ya maisha yetu ya kumshuhudia Bwana kwa ushujaa.

Bwana, utuhurumie!

- Baba yetu wa mbinguni, uwakumbuke wafuasi wote wa Mwanao waliotoa ushuhuda wa imani yao wakati wa vita na mashambulizi dhidi ya Kanisa lako.
- Mungu mkarimu, uwakumbuke waamini wote waaminifu ambao walitoa uhai wao kwa ajili ya wengine.
- Uwakumbuke, Baba mwema, wamisionari wote waliohubiri kwa furaha Habari Njema za Mwanao na kutoa uhai wao katika kazi hiyo.
- Uwakumbuke, Baba, waamini wote walioishi imani kwa ujasiri na ushujaa miongoni mwa maadui zao na wale wote waliopinga Jina la Yesu.
- Uwakumbuke, Mungu mwenye Huruma, wazazi wote waliofundisha watoto wao imani kwa uaminifu na upendo na kuwalea kama wakristo hodari katika Kanisa lako.
- Uwakumbuke, Baba mwingi wa rehema, waamini wote walioteswa na kudhihakiwa kwa ajili ya Imani yao.
- Uwakumbuke, Mungu wa Uzima, waamini wote waliotetea uhai wa mtoto ambaye hajazaliwa tangu sekunde ya kuumbwa kwake na kwa sababu hiyo walionewa na kuteswa.

Na sasa tusali kama Yesu alivyotufundisha kusali: Baba yetu…

Mungu, Baba yetu, uliyeweka msingi wa umoja, upatanisho na amani kwa njia ya Kifo cha Mwanao hapo alipojitoa sadaka kwa ajili ya wokovu wa wote na kutoa fidia kwa dhambi zote za dunia; tunakuomba, uliimarishe Kanisa lako linalokumbuka leo mashahidi wa imani wa vizazi vilivyotutangulia, walioosha mavazi yao katika Damu ya Mwanakondoo, ili mbele ya ulimwengu Kanisa lako ling’ae daima kwa nuru ya baraka zako, nasi utufanye kuwa mashahidi wa Yesu Mfufuka katika nyakati zetu hizi. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.
Kurudia Utume tuliopewa katika Sakramenti ya Kipaimara

Kiongoza-Ibada huanza kwa maneno yafuatayo au yanayofanana na hayo:

Ndugu zangu wapendwa, Katekisimu ya Kanisa Katoliki hutufundisha kwamba:

 “Matokeo ya adhimisho ambayo ni tunda la sakramenti ni mmimino wa pekee wa Roho Mtakatifu kama ulivyokuwa umetolewa tayari kwa mitume siku ya Pentekoste” (KKK, 1302). “Kutokana na ukweli huo Kipaimara huleta kukuza na kuzama kwa neema ya Ubatizo: 
  • kinatutia mizizi ndani zaidi katika kufanywa wana wa Mungu kunakotufanya tuseme “Abba, yaani, Baba”
  • kinatuunganisha kwa nguvu zaidi na Kristo
  • kinaongeza ndani yetu vipaji vya Roho Mtakatifu
  • kinakamilisha zaidi kiungo chetu na Kanisa
  • kinatupa nguvu ya pekee ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya kueneza na kutetea imani kwa maneno na matendo kama mashahidi kweli wa Kristo, ili kukiri kwa ujasiri Jina la Kristo na kamwe kutouonea aibu Msalaba: ‘kumbuka kwamba umepokea muhuri wa kiroho, Roho wa hekima na akili, Roho wa shauri na nguvu, Roho wa elimu na ibada, Roho wa uchaji mtakatifu, na ukilinde kile ulichokipokea. Mungu Baba amekutia alama na amejaza amana yake, Roho, moyoni mwako (Mt. Ambrose) (KKK,1303).

Wapendwa, sisi sote tulioalikwa kushiriki Ibada hii, tumekwishapokea neema ya Sakramenti ya Kipaimara. Tunajitahidi kuishi kwa nguvu ya neema hiyo siku kwa siku. Tunataka kuwa waaminifu kwa Roho Mtakatifu tuliyepewa siku ya Kipaimara. Roho huyo wa Bwana alitutia mafuta ya wokovu na kututuma twende kuihubiri Habari Njema kwa watu wote na kuwafanya kuwa wanafunzi wa Kristo. Roho Mtakatifu alituunganisha na Kristo na Kanisa lake kwa nguvu zaidi na kwa karibu zaidi. Kila mmoja wetu aliyepokea Sakramenti ya Kipaimara, alipokea pia utume wake kulingana na nafasi yake na wito wake ndani ya Kanisa la Kristo. Kila mmoja wetu aliyepokea Sakramenti hiyo, amekabidhiwa siku hiyo hatima ya Injili na Ekaristi katika ulimwengu tunamoishi. Kila mmoja wetu anawajibika katika Kanisa la Kristo kuhakikisha kwamba nafasi aliyopewa na Mungu katika Kanisa anaitumia kwa manufaa ya wote na kwa wokovu wa ulimwengu.

Katika Ibada hii ya Vijilia ya Sherehe ya Pentekoste, sisi sote tuliopokea Sakramenti ya Kipaimara, tunataka kutoa shukrani zetu za dhati kwa Mungu kwa tunu yenye thamani isiyopimika, yaani Sakramenti ya Kipaimara. Tunataka pia kumwomba Mungu ahuishe ndani ya kila mmoja wetu bidii ya kitume. Ndiyo maana nninamwuliza kila mmoja wenu:

Je, unafahamu kwamba katika Sakramenti ya Kipaimara Mungu Roho Mtakatifu alikutia mafuta ya wokovu na kukutuma kuikiri imani ya Kanisa, kuitetea na kuyaishi maisha yako kulingana na kanuni za imani? 

Nafahamu!

Je, uko tayari kuishi maisha yako ya kikristo kwa nguvu ya neema ya Sakramenti ya Kipaimara, ukihubiri Injili ya Kristo mbele ya mataifa, ukishiriki kikamilifu katika Liturujia ya Kanisa na kuwatumikia wengine kwa upendo wa kikristo?

Niko tayari!

Je, wataka kukua daima katika utakatifu, ukiishi kwa uaminifu wito uliopewa na Mungu katika Kanisa lake?

Nataka!

Mungu Mwenyezi, kwa nguvu ya Roho wako Mtakatifu, aihuishe upya neema mliyopewa katika Sakramenti ya Kipaimara. Awazidishie Roho wa hekima na akili, Roho wa shauri na nguvu, Roho wa elimu na ibada. Awajaze upya Roho wa uchaji mtakatifu. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

Amina!


Ibada ya kumalizia


Kiongoza-Ibada huwaalika waamini wainamishe vichwa vyao waipokee baraka kuu. Itumike baraka kuu ya Sherehe ya Pentekoste kutoka Misale ya Altare. Kisha ya baraka, Kiongoza-Ibada pamoja na wahudumu wote hutoa heshima kwa altare kwa kuiinamia. Wakati wa kurudi sakristia, wimbo wa Roho Mtakatifu (au wimbo wowote wenye ujumbe unaohamasisha uaminifu kwa utume utokanao na Kipaimara huimbwa).

No comments:

Post a Comment