Saturday, December 31, 2011

Wrapping Up


The time has come to wrap up this year of 2011. It has been my custom for many years now (after my late parish priest who used to do the same on the last day of each year) to present a report to the parochial community of the passing old year and projection of the incoming new year. Looking in retrospect with the grateful but also contrite heart, and looking ahead with hope in the heart and prayer on our lips - all wrapped in the form of the expose or the annual report of the state of the matters and our plans for the imminent future... 


I have just finished celebrating the Thanksgiving Mass with my parochial community and I would like to share with swahili speaking readers of my blog (hoping that google translator works also with swahili so all other readers may get the message as well) the text of the report I have just presented to my parishioners. So, here it is in extenso. And it is my hope that our concerns, hopes and achievements may become a food for thought for all of you too. God bless us all as we enter the new year with hope in our hearts and rock solid faith in our Merciful God. I wish you all a prosperous, blessed and successful New Year 2012!


Homilia ya Misa ya Shukrani ya kufunga Mwaka 2011 
na kukaribisha Mwaka Mpya wa 2012
Hekalu la Huruma ya Mungu, 31.12.2011, saa 11.00 jioni
Furahini sikuzote, ombeni bila kukoma, shukuruni kwa kila jambo, 
maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu” 
(1 Tes 5,16-18)
Wapendwa wanaparokia ya Kiabakari!
Tumekusanyika jioni hii, siku ya mwisho ya mwaka wa 2011, katika Hekalu hili la Huruma ya Mungu, ambalo ni Kituo cha Kijimbo cha Hija ya Huruma ya Mungu tukisukumwa na hitaji moja – kutoa shukrani zetu za dhati kwa Mwenyezi Mungu na kumwambia – Asante sana! – kwa mema yote aliyotujalia katika kipindi cha mwaka huu wa 2011; pia kutamka kutoka ndani ya kilindi cha mioyo yetu iliyovunjika na kupondeka – „Baba, utusamehe kwa maana tumetenda dhambi!” 
Tunapofanya hivi kama familia ya Watoto wa Mungu, inatupasa kukumbuka kwamba tumemaliza hivi karibuni Mwaka wa Jubilei ya Miaka 100 ya Ukristo katika Jimbo letu la Musoma. Tunahama mwaka huu wa 2011 na kuhamia mwaka mpya wa 2012 kupitia kwa mlango ambao ni Yesu wa Ekaristi na kuipokea zawadi ya muda wa miezi 12 mipya katika safari ya maisha yetu – tuweze kwa baraka zake kuitumia zawadi ya muda wa mwaka mpya jinsi Mungu Baba anavyotaka mwenyewe.
Basi wapendwa, tusonge mbele kwa matumaini tukitegemea msaada wake Kristo, Mwana wa Mungu, aliyetwaa mwili  wa kibinadamu Milenia mbili zilizopita kwa ajili ya upeo wa upendo wa Mungu Baba kwetu sisi wanadamu.  Tunahitaji macho ya uchambuzi kutambua uwepo wake kati yetu katika Kanisa lake Takatifu. Zaidi ya yote tunahitaji moyo mkarimu tukubali kuwa vyombo vya kazi yake. Je, hatukuadhimisha Mwaka wa Jubilei ya Miaka 100 ya Ukristo kwa lengo la kuhuisha upya uhusiano wetu na huyo Kristo aliye chimbuko la tumaini letu? Je, hatukuingia Milenia ya Tatu tukiwa na nia thabiti ya kuchochea upya moto wa Injili katika dunia yetu, na hasa katika mazingira tunamoishi? Sasa, Kristo ambaye tumemtafakari na kumpenda  upya katika fumbo la Ekaristi, anatuamuru tukaanze tena safari yetu. “Nendeni basi, mkawafanye watu wa mataifa yote wawe wafuasi wangu; wabatizeni kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu” (Mt 28:19). Agizo hili la kimisionari linatuhimiza tuwe na ari kama wale Wakristo wa kwanza kabisa. Na tunaweza tukaiaminia nguvu ya Roho yule yule aliyemiminwa siku ile ya Pentekoste. Ndiye anayetusukuma hata leo, tuanze upya tukitegemezwa na tumaini ambalo haliwezi kutuhadaa (Rum 5:5).
Katika safari yetu hii, tunasindikizwa na Mama Bikira Maria Mtakatifu, Mama wa Mungu, Somo wa Kanisa Kuu na Jimbo letu la Musoma. Sasa nawaelekeza tena kwa Maria aliye “Pambazuko Angavu la Wokovu” na „Kiongozi amini wa safari yetu ya kwenda mbinguni”. Kwa mara nyingine tena, nikirudia maneno ya Yesu mwenyewe, na nikitamka maneno yanayoeleza “Pendo la kimwana” la Kanisa lote, ninamwambia Mama Maria: “Mama, watazame wanao” (rej. Yn 19:26).

I - SHUKRANI KWA MAFANIKIO YA KICHUNGAJI
  1. Nasimama mbele yenu, Waamini wenzangu, kumshukuru Mungu mwenye Huruma kwa mema yote aliyotujalia mwaka huu wa 2011. Tumshukuru Mungu kwa dhati kwa mema hayo yote yasiyohesabika!
  2. Tutafakari kidogo juu ya matukio ya mwaka huu katika maisha ya Parokia yetu na maisha yetu binafsi. Kwa ajili ya mema gani tunapaswa kumshukuru Mungu leo katika ibada hii ya mwisho kabisa ya mwaka huu wa 2011? Binafsi, naona ni vema kutaja mambo muhimu machache kati ya mengi ambayo kwayo tumshukuru Mungu kwa moyo wote:
  1. Kwanza, tunakushukuru Mungu Baba kwa kumtangaza Baba Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Mwenye Heri na kutujalia tunu bora ya Masalia Matakatifu ya damu yake tuliyokabidhiwa na Mwadhama Kardinali Stanislaw Dziwisz kwa ajili ya Kituo cha Kijimbo cha Hija ya Huruma ya Mungu.
  2. tumshukuru Mungu kwa neema ya kufanikisha maadhimisho mbalimbali ya Mwaka wa Jubilei ya Miaka 100 ya Ukristo katika Jimbo letu,  
  3. Shukrani kubwa kwa Mungu kwa kutujalia neema ya kufanikisha hija za vikundi mbalimbali katika kituo hiki cha kijimbo cha hija – hasa siku ya Sherehe ya Huruma ya Mungu na wakati wenzetu wa Butiama walipohiji hapa mwezi wakitembea kwa mguu kutoka Butiama.
  4. Tumshukuru Mungu kwa zawadi ya Jimbo jipya la Bunda na Askofu wake wa kwanza, Mhashamu Renatus Nkwande,
  5. Asante sana, Baba mwema, kwa neema zako nyingi ulizotujalia katika kipindi chote cha mwaka wa 2011, hasa kwa njia ya Sakramenti na Ibada zilizoadhimishwa katika Parokia yetu, katika Hekalu hili, vigangoni na katika jumuiya zetu; kwa Wakristo wapya waliobatizwa mwaka huu na walipokea Komunyo ya Kwanza; kwa ndoa takatifu zilizofungwa mwaka huu, kwa waamini waliotumia mara kwa mara Sakramenti ya Kitubio kujipatanisha na Mungu na kurudishiwa heshima ya kuwa tena watoto wapendwa wa Mungu waishio katika hali ya neema ya utakaso; kwa wagonjwa wetu waliopenda kukutana na Yesu mwenye Huruma katika ugonjwa wao. Kwa kifupi, kwa mema yote aliyotujalia Mwenyezi Mungu mwaka huu katika Liturujia ya Kanisa na katika huduma mbalimbali za kichungaji.
  6. Kwa nafasi zote za kuweza kuadhimisha Ibada mbalimbali tukiongozwa na Mhashamu Askofu wa Jimbo letu, Michael Msonganzila na hasa alipokuja kuadhimisha Sherehe ya Huruma ya Mungu.
  7. Ninamshukuru Mungu kwa kunijalia afya ya kutosha katika mwaka huu na kupata msaada katika matatizo ya kiafya wakati wa safari yangu ya mwezi wa tisa, 
  8. Asante, Mungu Baba, kwa misaada mbalimbali ya Mapadre wa Butiama, Zanaki, Makoko Seminari na kutusaidia katika nyakati mbalimbali kila tulipowahitaji. Ninamshukuru hasa Mheshimiwa Padre Godfried Maruru aliyesimamia Parokia wakati sipo na wakati wa Noeli mwaka huu. 
  9. Mungu ashukuriwe kwa huduma mbalimbali za kiroho, kichungaji, kiafya na kielimu zinazotolewa na Watawa wetu, Masista wa Shirika la Watumishi Wadogo wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, katika Parokia yetu na taasisi zake,
  10. Tumshukuru Mungu kwa wito wa kitawa wa makandidati waliojitokeza kujiunga na Shirika la Watawa wetu,
  11. Yesu, Mchungaji Mwema, tunakushukuru kwa safari ya wito ya vijana wetu, Fratera Augustino Mapambano na waseminari wadogo.  
  12. Mungu Baba, pokea shukrani kwa kazi mbalimbali za Makatekista wetu ambao walisimamia kazi za katekesi vizuri na kuendeleza vema utume wao jinsi inavyotakiwa.
  13. Asante, Mungu Mwenyezi, kwa neema ya kufanya kazi za kichungaji kwa ushirikiano mzuri na wa karibu sana na Halmashauri ya Walei Katoliki ya Parokia na kwa namna ya pekee na Viongozi wa Kamati Tendaji ya HWK Parokia ambao wamekuwa msaada mkubwa katika kutekeleza majukumu yangu kama Paroko. Tunamshukuru Mwalimu Patrice Magoti, aliyehama Parokia kurudi nyumbani Tarime, kwa uongozi wake mzuri wa muda mrefu. Tunamtakia afya njema na baraka katika maisha yake na utume huko aliko Tarime.
  14. Mungu mwema, tunakushukuru kwa utume wa wasalishaji wetu waliotimiza kwa uaminifu huduma takatifu.
  15. Ninamshukuru Mungu kwa vyama vyote vya kitume vya Parokia kwa uwepo wao na kazi zote za kiroho walizoweza kuzifanikisha katika kipindi cha mwaka mzima.
  16. Ninamshukuru Mungu kwa upendo wa wakristo kwangu, Paroko wenu, kwa moyo wa kuniombea na kuwa tayari kunisaidia kwa kila hali, kwa matoleo ya vipaji vya Misa na ukarimu wao. Mungu awarudishie mara elfu upendo na ukarimu wao kwetu!
  17. Asante, Mungu Baba, kwa baraka zako zote ulizowajalia wafanyakazi na wagonjwa katika kituo chetu cha afya, kwa huduma nzuri zilizotolewa kituoni mwaka huu na usimamizi mzuri wa kituo wa Mhe. Sista Grace Mukupa na wasidizi wake. 
  18. Tunakushukuru Mungu kwa uwepo wa Kituo cha Elimu na Malezi cha Mwenye Heri Yohane Paulo II katika Parokia yetu, na taasisi zake zilizopo kwa sasa - Shule ya Awali na Shule ya Msingi. Tunakushukuru kwa usimamizi mzuri wa Mkuu wa Kituo, Mhe. Sista Mary Chongo, kazi nzuri ya Masista na walimu na wafanyakazi wote.
  19. Asante, Mungu mwema, kwa ukarimu wa waamini na wafadhili wetu ndani na nje ya nchi waliochangia maendeleo ya Parokia katika miradi, misaada, harambee mbalimbali na katika michango mingine. Kutokana na ukarimu wao huo tulifanikisha kukamilisha madarasa mawili katika shule yetu ya msingi pamoja na meza na viti vya wanafunzi; tulinunua vitabu vya shule kwa darasa la kwanza na la pili; tulikamilisha ujenzi wa tenki kuu ya maji, tulikamilisha ujenzi na kuweka samani katika konventi ya Mt. Gemma Galgani ya masista wetu; tulijenga bafu mpya katika chumba kimojawapo cha wageni, tulinunua na kusimika matenki saba ya maji ya mvua katika nyumba ya mapadre, nyumba ya masista na katika kituo cha afya na kufanya kazi nyingine ndogondogo za kimaendeleo.
  20. Asante, Baba, kwa kazi nzuri ya wafanyakazi wa Parokia ambao walifanya kazi kwa moyo mmoja na kwa upendo kwa Parokia yao. Tunawashukuru na kuwatakia heri na baraka katika ajira yao mwakani. 
  21. Asante, Mungu mwema, kwa Waamini wanaofika kushiriki Misa za kila siku walioongoza sala za asubuhi kanisani humu kila siku mwaka huu kwa uaminifu mkubwa kabisa. Na kwa huduma za vyama vyote vinavyohusika na liturujia ya Kanisa Kuu. Kwa ujumla wahusika hao wote – Wasomaji wa Neno, Wanawito wavulana na wasichana, Utoto Mtakatifu na Kwaya zote wamejitahidi mwaka huu kuwa waaminifu zaidi kwa kanuni za kiliturujia kuliko miaka ya nyuma - hali inayotakiwa katika Kituo cha Kijimbo cha Hija.
  22. hatimaye, Mungu mwema wa walio hai, tunakushukuru kwa kuturuhusu kuendelea kuishi katika ulimwengu huu kwa kuendelea kutupa afya ya kutosha, kwa kutujalia tudumu katika Ukristo. Mungu Baba, asante sana! Nao ambao ulipenda kuwaita kwako mwaka huu, tunakuomba uwapumzishe katika amani yako huko mbinguni. Raha ya milele uwape, ee Bwana… Wapumzike kwa amani. Amina!
  1. Ndugu zangu wapendwa, yapo mambo mengi sana yasiyohesabika ambayo kwayo tunapaswa kumshukuru Mungu kupitia kwa Mama Bikira Maria, Somo wa Jimbo letu la Musoma, lakini kwa haya machache ninamshukuru Mungu zaidi na kwa dhati kabisa. Nawakaribisheni pia, wapendwa, kila mmoja wenu afanye mahesabu ya mema yote aliyojaliwa na Mungu mwaka wa 2011 na kumshukuru Mungu kwa dhati kabisa!
  2. Pamoja na shukrani zangu za dhati kwa Mungu na kwa wote niliowataja mimi binafsi, bado tunahitaji kumwomba Mungu msamaha kwa dhambi na makosa tuliyoyatenda katika kipindi cha mwaka huu wa 2011. Kila mmoja wetu kwa kutafakari mwenendo wa maisha yake mwenyewe, akisaidiwa na mwanga wa Roho wa Bwana ataweza kutambua makosa yake binafsi na kuomba radhi kwa Mungu na kwa wale aliowakosea. Nami mwenyewe, kwa kufuata desturi yangu ya siku zote, ninasimama mbele yenu siku ya mwisho ya mwaka kuomba radhi kwa makosa yoyote yale ambayo katika kutekeleza majukumu yangu ya kichungaji kama Paroko inawezekana niliwakosea tangu mwaka uanze hadi sasa. Naomba msamaha kwa kila mmoja ambaye kwa namna moja au nyingine sikumtimizia haja zake halali au nilishindwa kumuonyesha upendo alioustahili. Pia, ninapenda kutamka kwamba kama mtu binafsi, nikiwa mwanadamu na mkristo mwenzenu, nawasamehe wote walionikosea kwa njia yoyote ile na kuninyima upendo na heshima ninayostahili au walikusudia kunitendea mabaya mwaka huu. 
II - MATATIZO YALIYOJITOKEZA MWAKA HUU WA 2011
Katika matatizo kadhaa yaliyokuwa yamejitokeza mwaka huu katika Parokia yetu, katika mtazamo wangu ningependa kuyataja machache tu yafuatayo:
  1. Elimu duni ya waamini na viongozi walei kwa upande wa teolojia ya Kanisa (ecclesiology), muundo wake, Mapokeo ya Kanisa, Sheria ya Kanisa, Hati mbalimbali za Kanisa, uwajibikaji katika Kanisa, mipaka ya uongozi na nafasi ya walei katika Kanisa. Tatizo hili linahitaji ufumbuzi wa kina na wa muda mrefu wa kutosha. Katika malengo yetu ya kichungaji swala hili litapewa kipaumbele.
  2. Elimu duni ya Biblia na matini za liturujia na sheria zinazotawala liturujia ya Mama-Kanisa. 
  3. Elewa ndogo ya waamini kuhusu taratibu za JNNK na ushirika hafifu wa wanaparokia wengi katika maisha ya kila siku ya JNNK zao. Wengi hudhani kwamba kipimo cha kuwa mwanajumuiya hai ni kushiriki ibada za jumatano tu na si maisha yote ya jumuiya na moyo wa ujirani mwema wa kila siku.
  4. Tatizo kubwa la JNNK ni uhaba wa wasilishaji wetu tuliowaandaa miaka ya nyuma. Katika vipaumbele vya mwaka wa 2012 ni kuwaendeleza zaidi wasalishaji wetu na kuwapata wapya.
  5. Hali ya kuyumba kwa baadhi ya Vyama vya Kitume katika Parokia. Mwakani tutalivalia njuga swala la kuvisaidia vyama hivyo. 
  6. Katekesi ni kazi ya kwanza ya Mapadre na ni jukumu la viongozi walei kuhakikisha kwamba mafundisho ya dini kwa walei wenzao yanatolewa kadiri ya miongozo ya Kanisa tena kwa ufanisi mkubwa. Tutaendelea kuweka Idara ya Katekesi katika mfumo mzuri na kuilea kwa karibu sana katika kipindi cha mwaka wa 2012. 
  7. Kwa upande wa mafundisho ya dini, hali ya kufundisha dini katika shule za msingi katika Parokia si nzuri hata kidogo. Si ajabu, maana hatujaunda UWAKA Parokiani na idadi ya Makatekista ni ndogo. Haikidhi mahitaji. Uhaba wa makatekista si jambo jema hata kidogo. Lakini, kama Balozi wa Papa alivyomwambia Baba Askofu wetu siku moja – „Baba Askofu, najua una uhaba wa Mapadre. Lakini usiwe na papara, usipadrishepadrishe eti, kuziba mapengo. Afadhali kuwa na Mapadre wachache kuliko kumpadrisha mmoja ambaye hafai na atavuruga Kanisa lako”. Kumbe, tuna wajibu wa kuwatafuta na kuwaanda Makatekista wapya na wa kutosha kukidhi mahitaji ya Kanisa. 
  8. Maisha ya kiroho na kisakramenti. Matatizo ni mengi hapa. Familia nyingi sana hazisali pamoja. Utoto Mtakatifu ni ukombozi katika swala hili. Watoto wanakuwa wamisionari kwa wazazi wao wenyewe. Waamini wengi wa Dominika walizoea kukomunika katika hali ya dhambi bila kuungama kwa muda mrefu au hawaungami kabisa. Ni tatizo kubwa sana. Dhambi hii hutukosesha neema nyingi. Kila dhambi na hasa dhambi za kukufuru sakramenti, kuvuruga ibada na kukosa maadili tukiwa ndani ya nyumba ya Mungu ni jiwe shingoni kwa kila mkristo. Ni mzigo unaotulemaza. Dhambi ya mmoja inawahusu wote. Pengine tunasahau hilo. Waamini wachache wanatumia sakramenti ya Kitubio ukilinganisha na idadi ya wanaokomunika. Hii inaonyesha huenda mafundisho hafifu waliyoyapata walipokuwa wanasoma. Sielewi nani aliwaambia kwamba wakishapokea Komunyo ya Kwanza, ni ruksa kukomunika maisha yao yote bila kujali wanastahili au la, wana dhambi au la. Zaidi! Wana kikwazo au la! Ndoa chache sana zinafungwa ukilinganisha na idadi ya wakristo wanaochukuana na kuanza maisha ya pamoja ya kimada au kwa kufuata mila na desturi tu (ndoa za kienyeji). Ndoa za jumla si dawa. Kanisa haliwezi kuwa imara kama familia katoliki hazipo au ziko chache au zinayumba.
  9. Kwa upande wa maisha ya kiroho, asilimia kubwa ya wanafunzi wa shule za msingi na vijana, baada ya kupokea Komunyo ya Kwanza hawaungami kabisa au mara chache sana (labda wakati wa sikukuu) mpaka wapokee Kipaimara na kuhamasishwa waungame kabla ya kupokea sakramenti hiyo. Wanawito wa kiume na wa kike nao wanayo tabia hii mbaya. Hivyo, wazazi wa kimwili na kiroho hawana budi kuwasindikiza vijana wao katika safari ya kiroho na kuhakikisha kuwa wanaungama kila Ijumaa ya Kwanza ya mwezi. Watafaulu katika jambo hili endapo wazazi wenyewe watakuwa mfano kwa vijana wao katika kuungama mara kwa mara.
  10. Tatizo jingine ni imani za kishirikina za waamini wetu zinazojionyesha katika elewa yao ya Sakramenti za Kanisa na visakramenti vyake. Kila siku tunashuhudia foleni ya watu wanaochota maji ya baraka kabla au baada ya Misa, lakini hatuwaoni wakijipanga katika foleni kwenda kuungama. Picha za Yesu, Maria na Watakatifu zinabarikiwa kila kukicha, kitabu cha mawaridi ya sala kina soko kubwa wakati hakina idhini ya Kanisa maana ni mkusanyo wa sala ambao unamfanya mwamini apate imani kwamba akisali sala fulani atapewa moja kwa moja neema fulani (na wazo hili linafanana na imani ya kishirikina!), rozari za kila muundo zinaletwa zibarikiwe (wengine wanadai eti, rozari ibarikiwe kila mwaka, eti baraka yake inaexpire), na papo hapo Sakramenti za Kanisa ambazo zinatukutanisha na Yesu mwenyewe zimewekwa kando. Tunaamini zaidi vitu, visakramenti kuliko nguvu za Yesu mwenyewe zinazopatikana katika Sakramenti, hasa Kitubio na Ekaristi Takatifu.
  11. Waamini wengi bado hawajawa na desturi ya kuabudu Ekaristi Takatifu nje ya baraka na ibada. Hawajawa na desturi hai ya kumtembelea Yesu wa Ekaristi siku za katikati ya wiki kwa ajli ya sala na tafakari. Wito wangu kwa kila mwanaparokia – msimwache Yesu peke yake katika tabernakulo.
  12. Ukarimu katika parokia bado ni shida. Hasa ulipaji zaka na matoleo mbalimbali kwa ajili ya kulitegemeza Kanisa na Parokia. Waamini hawaelewi kuwa zaka ni amri ya Kanisa, ni fungu kumi la pato la mwamini, si hiari yake. Tatizo hili linahitaji katekesi ya kina na ya muda mrefu. Kulipa zaka kunamfanya mwamini kuwa mwanakanisa hai ambaye – endapo hana kikwazo kingine – ana haki ya kupata huduma zote katika Kanisa lake. Asiyelipa zaka si mwanakanisa. Anaweza kuwa mtu wa dini, lakini kamwe mwanakanisa, maana anakataa kulitegemeza. Tatizo jingine ni kukosa moyo wa shukrani kwa Mungu kwa wanaparokia wengi. Bahasha za Noeli, za Pasaka, shukrani ya mavuno na shukrani binafsi kwa mfano kwa kuomba Misa za kumshukuru Mungu kwa ajili ya kupata fadhila fulani - hapo kuna shida kubwa.
III - MATARAJIO YA MWAKA WA 2012
  1. Kutatua matatatizo yaliyoorodheshwa hapo juu
  2. Kutekeleza na kufanikisha kalenda ya kichungaji ya Parokia ya 2012
  3. Kuadhimisha kikamilifu Jubilei ya Miaka 20 ya Parokia ya Kiabakari na Miaka 15 ya kutabarukiwa kwa Hekalu la Huruma ya Mungu,
  4. Kukarabati Hekalu hili la Huruma ya Mungu – ndani na nje pamoja na mnara wake.
  5. Kuendelea kukamilisha shule yetu na kuzungushia uzio shule yetu ya awali.
  6. Kuendeleza Kituo chetu cha Afya - vifaa vya kisasa pamoja na mawodi ya wagonjwa.
  7. Kutafuta ufadhili ndani na  nje ya parokia kwa ajili ya ujenzi wa vigango vya Parokia,
  8. Kujenga jengo la ofisi za Parokia kati ya kanisa na nyumba ya Mapadre,
  9. Kuendeleza mandhari ya Mlima wa Huruma ya Mungu, 
  10. Kuanzisha upya mradi wa ufugaji na kilimo,
  11. Kuendelea kutekeleza Dhima ya Kichungaji ya Parokia 2002-2012 (ninaomba viongozi wote waisome na kuielewa ili twende pamoja katika utekelezaji wake)
  12. Kuimarisha Halmashauri ya Kichungaji ya Parokia – ambayo ni kielelezo cha Taifa zima la Mungu na uwakilishi wake – Mapadre, Watawa na Waamini Walei; kwa namna ya pekee kuhusisha zaidi kamati mbalimbali za HK Parokia katika maisha ya kila siku ya Parokia na mahitaji yake ya kichungaji
  13. Kuimarisha Halmashauri ya Walei Katoliki ya Parokia kadiri ya mwongozo wa Kanisa
  14. Kuimarisha Caritas Parokia na kuunganisha juhudi za wote – katika mfumo mmoja unaoeleweka wa Caritas Parokia
  15. Malezi endelea ya JNNK 
  16. Semina za wasalishaji, makatekista na viongozi walei
  17. Kuimarisha Idara ya Katekesi 
  18. Kuimarisha financial policy parokiani tangu JNNK hadi Parokiani
  19. Kampeni ya zaka Parokiani, bahasha za Pasaka na Noeli pamoja na Misa za shukrani – uhai wa kiuchumi wa Parokia hutegemea kwa kiasi kikubwa uwajibikaji wa waamini wote katika kulitegemeza Kanisa 
  20. Mafungo ya Kuamsha Imani kabla ya ziara ya Baba Askofu,
  21. Kuandaa ziara ya kichungaji ya Baba Askofu Parokiani.
  22. Kuanza mchakato wa maandalizi ya Jubilei ya Miaka 50 ya Ukatekista wa Mwalimu Benjamin Ndege, Jubilei ya Miaka 25 ya Upadrisho na Miaka 50 ya Kuzaliwa kwa Paroko na Upadrisho wa Fratera wetu Agostino Mapambano - matukio haya yote ni mwaka 2013.
  1. HITIMISHO 
Hatimaye, tumkabidhi Mama yetu, Maria Mtakatifu, Mama wa Mungu, hatima ya Parokia yetu katika mwaka wa 2012. Tujikabidhi kwake, tuzikabidhi familia zetu, tuukabidhi wokovu wa kila mmoja wetu na kila mmoja anayeishi ndani ya mipaka ya Parokia yetu – awe mkatoliki, asiwe mkatoliki. Mama Maria kwa maombezi yake na usimamizi wake bora atufikishe sote salama nyumbani kwa Mungu Baba wa mbinguni. Amina.
Asanteni kwa kunisikiliza!
Pd. Wojciech Adam Koscielniak
Paroko
31/12/2011

2 comments:

  1. Happy New Year dearest Wojciech and may all your plans for 2012 come to fruition. I got the 'gist' of your homily using google although it is not that precise. As always you are so full of gratitude and so humble as you thank God for all the blessings you and your community received. You have a very comprehensive plan for what has to be done in 2012 and I wish you all the best in its implementation . Quite a busy schedule ahead but don't forget the time needed to recuperate yourself and keep well. May 2012 be one of the best years so far and may all your dreams be realised. With affection and love from all the Daly clan as we make the transition from this year to the next full of expectations and hope. Lena

    ReplyDelete
  2. I know that myself cannot do anything good. So today I knelt down in front of the altar and said a prayer of consecration of the whole parochial community to the maternal care of Our Lady. I know too well that challenges of this year are massive, they look a bit intimidating but after today's consecration I feel much more secure and confident that we will manage somehow and that the Lord's will be done... Gos bless you much, Lena dear, Tom and the Clan. Praying for you always with pride and gratitude...

    ReplyDelete